Kibiti Mambo Mazito Hadi Sasa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga

Kwa ufupi

Hadi sasa idadi ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi tangu mauaji mkoani Pwani yaanze imefikia 38

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kibiti/Dar. Adui anayeua askari, viongozi wa Serikali za Mtaa na wananchi katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani ambaye sasa nchi nzima inamsaka, bado ni kitendawili.

Kitendawili hicho hakijateguliwa kwa kuwa usiku wa kuamkia jana, mkazi mmoja wa Kitongoji cha Nyambwanda katika Kijiji cha Hanga wilayani Kibiti, Hamis Ndikanye (54) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.

Tukio hilo linafanya idadi ya watu ambao wamekwishauawa kwa kupigwa risasi tangu mauaji mkoani Pwani yaanze kuripotiwa na kuvuta hisia za Watanzania Januari 2015 kufikia 38. Kati ya hao, 13 ni askari polisi ambao wameuawa tangu Februari mwaka huu.

Katika tukio hilo la usiku wa kuamkia jana, Hamis Saidi ambaye ni ndugu wa marehemu amesema watu hao wanaodhaniwa kuwa watano wakiwa na bunduki walifika nyumbani kwa Ndikanye saa sita usiku na kufanya mauaji hayo.

Amesema watu hao baada ya kufika nyumbani kwa ndugu yake, waligonga mlango wa nyumba yake wakimtaka afungue lakini aligoma.

Amesema wahalifu hao waliamua kuvunja mlango huo kwa kitu kizito na kisha kuingia ndani na kumkuta Ndikanye akiwa amelala na mkewe.

Saidi amesema kabla ya kufanya mauaji hayo ya nduguye, wahalifu hao walimfunga mkewe kwa kitambaa usoni na mikononi, kisha kumpiga marehemu risasi mbili zilizosababisha kifo chake.

Mganga wa Kituo cha Afya Kibiti, Dk Sadock Bandiko amesema katika uchunguzi alioufanya kwenye mwili wa marehemu, alikuta majeraha wawili yaliyotokana na kupigwa risasi mbili, moja kichwani na nyingine mgongoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji, Onesmo Lyanga (pichani) amesema tayari polisi wamekwenda Nyambwanda kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.

Comments

Popular posts from this blog

Taarifa Kuhusu Kupotea Kwa Msanii Roma Mkatoliki.

Taarifa Kuhusu Mgomo wa Mabasi.